Find us on facebook

Pages

Follow Me.

Thursday, June 6, 2013

WAPIGANAJI WA MAU MAU SASA KULIPWA.

Uingereza imekubali kuwalipa maelfu ya Wakenya shilingi bilioni
1.8 za Kenya kama fidia kwa mateso waliyofanyiwa na wanajeshi wa Uingereza wakati wa vuguvugu la Mau Mau kati ya mwaka 1952 na 1960, wakati utawala wa Muingereza ulipokaribia kufikia ukingoni nchini humo. Hayo ni kwa mujibu wa kauli zilizotolewa jana na wakili na shahidi.
Mazungumzo baada ya mahakama ya jijini London kuamua mwezi Oktoba mwaka jana kwamba wazee watatu Wakenya, waliohasiwa, kubakwa na kupigwa wakati walipokuwa kizuizini wakati wa ukandamizaji wa vikosi vya Uingereza na washirika wao wa Kenya katika miaka ya 1950, wangeweza kuishitaki serikali ya Uingereza.
Mateso hayo yalifanyika wakati wa kile kilichojulikana kama utawala wa hatari kati ya mwaka 1952 na 1960, wakati wapiganaji wa Vuguvugu la Mau Mau walipoyashambulia maeneo ya Uingereza, na kusababisha hofu miongoni mwa wazungu waliokuwa wakiishi nchini Kenya na kuitia wasiwasi serikali ya mjini London.
"Tumekubaliana kufikia maelewano nje ya mahakama," alisema wakili Paul Muite, mshauri wa wapiganaji wa zamani wa kundi la Mau Mau wanaotaka kulipwa fidia. Akizungumza na shirika la habari la Reuters, bwana Muite pia alisema kuwa mazungumzo hayo yalimjumuisha kila mtu aliyekuwa na ushahidi wa kutosha wa mateso. "Na idadi hiyo ni takriban 5,200," alisema Muite lakini akasita kutaja kiwango cha fedha kitacholipwa kama fidia.
Tangazo rasmi linatarajiwa kutangazwa leo (06.06.2013). Afisi ya Uingereza inayohusika na masuala ya kigeni imekataa kutoa tamko kuhusu taarifa kwamba fidia hiyo ingefikia jumla ya paundi milioni 14 za Uingereza. Hii ina maana kila Mkenya anayedai fidia atalipwa kiasi cha paundi 2,600 au shilingi 339,560 za Kenya.Vuguvugu la Mau Mau lilianzishwa katika miaka 1950 miongoni mwa jamii ya Wakikuyu wa Kenya. Wafuasi wake waliunga mkono mapambano kama njia ya kupinga utawala wa Muingereza katika taifa hilo. Tume ya Haki za Binaadamu ya Kenya imekadiria kwamba Wakenya 90,000 waliuwawa au kulemazwa, na wengine 160,000 wakawekwa vizuizini wakati wa vuguvugu hilo, akiwemo babu wa rais wa Marekani, Barack Obama. Wapiganaji wa Mau Mau ambao sana sana walikuwa na nywele ndefu na kuvalia ngozi za wanyama kama nguo, walizivamia jamii za wakoloni.
Uingereza ilijaribu kuizuia kesi ya Mau Mau
Uingereza ilijaribu kwa wiki tatu kuwazuia wapiganaji wa zamani wa Mau Mau kwenda mahakamani, hatua iliyosababisha ukosoaji mkubwa kutoka kwa wahanga wazee waliopigania uhuru. Wazee hao waliishutumu serikali ya Uingereza kwa kujaribu kutumia vipengee vya kisheria kukabiliana na kesi hiyo.
Caroline Elkins, profesa wa historia katika chuo kikuu cha Havard aliyekuwa kama shahidi mtaalamu katika kesi hiyo iliyoanza mnamo mwaka 2009, amesema maafikiano ya kuwalipa fidia Wakenya hao yatakuwa ya kwanza ya aina yake katika Himaya ya zamani ya Uingereza. "Utaonekana kama ushindi," ameliambia shirika la habari la Reuters wakati wa ziara yake mjini Nairobi ambako amekwenda kwa ajili ya tangazo la Uingereza. Elkins aliandika kitabu kwa jina "Imperial Reckoning: The untold Story of Britain's Gulag in Kenya" ambacho kilitumiwa kama msingi wa kesi ya Mau Mau.
Uingereza ilisema dhamana ya matukio wakati wa vuguvugu la Mau Mau yalikabidhiwa kwa Kenya baada ya uhuru mwaka 1963, hoja ambayo mahakama za mjini London ziliikataa. Serikali ya Uingereza baadaye ilisema madai ya wapiganaji hao wa Mau Mau yaliwasilishwa kuchelewa kwa mujibu wa sheria. Lakini jaji katika kesi ya Oktoba mwaka jana alisema kuna ushihidi wa kutosha wa kimaandishi kuwezesha kesi ya haki kufanyika.
Mwandishi: Josephat Charo/RTRE
Mhariri: Mohammed Khelef

No comments:

Post a Comment