kufanya mazungumzo na kikundi cha upinzani cha FDLR, ili kumaliza uasi nchini humo.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, ametoa msimamo huo jana, wakati akijibu hoja za wabunge waliojadili hotuba ya bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka 2013/2014.
Membe, alisema siku sita zilizopita, Rwanda ilitoa tamko la kupinga ushauri uliotolewa na Rais Kikwete Mei 26, mwaka huu, alipohudhuria maadhimisho ya miaka 50 ya Umoja wa Afrika (AU) huko Adis Ababa, Ethiopia.
Alisema Rais Kikwete, alitoa ushauri huo kwa sababu Rwanda ina vikundi visipopungua 20, vinavyopigana ndani ya misitu ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (RDC).
Alisema wakati vikundi hivyo vikiendelea kupambana, kikundi kikuu cha uasi huko DRC, M23,
kinaendelea na mazungumzo na serikali ya Rais Joseph Kabila nchini Uganda.
Rais Kikwete alipendekeza kwa Rais wa Rwanda, Paul Kagame, kufanya mazungumzo ya amani na upinzani.
Membe, alisema Rais Kikwete alitoa ushauri huo kwasababu nchi hiyo imekuwa ikijaribu kupigana na upinzani (FDLR) kwa miaka 16 iliyopita bila mafanikio.
“Kama suluhisho la kuondoa upinzani Rwanda ni vita, wamefanya hivyo kwa miaka 16 wameshindwa na kwa hiyo Tanzania yenye uwezo wa kufanya mazungumzo haya kwa amani katika nchi za Burundi, Rwanda, Congo, Zimbabwe na Angola, tukawashauri wenzetu kwa nia njema,” alisema.
Hata hivyo, alisema badala yake, serikali ya Rwanda, imetoa tamko la kutaka iombwe radhi, kwa madai kuwa Rais Kikwete `amefanya matusi’ kwa kuwa hawawezi kuongea na wauaji.
Membe alimnukuu Waziri Mkuu wa zamani wa Israeli, Isaack Rabin, Novemba mwaka 1995, aliposema, ‘tunajenga amani na tunajadiliana na madui wetu na si marafiki’.
“Naomba kama serikali ya Rwanda inanisikia, wafanye mazungumzo ya amani na maadui, wasingoje kufanya mazungumzo ya amani na Tanzania ambao ni marafiki, unaepuka nini,” alihoji.
Aliongeza, “kama Taifa la Israel na Palestina wanazungumza, wewe ni nani unakataa kufanya mazungumzo. Mtapigana hadi lini kama miaka 16 mmeshindwa.”
Membe alihoji na kusema,” wanaona aibu gani kufanya mazungumzo na upinzani, ningependa serikali ya Rwanda ijue kuwa kwa tabia yetu tangu uhuru tunatoa kipaumbele kwa mazungumzo ya amani.” Membe alisema hata Tanzania ilipopeleka majeshi DRC, bado msisitizo ulikuwa katika kumhimiza msuluhishi wa mgogoro wa DRC, Rais Yoweri Museveni, afanikishe mazungumzo ya pande zinazopingana.
Alisema iwapo Rwanda hawautaki ushauri huo, wanapaswa kuuacha badala ya kuibua madai ya kutaka waombwe radhi.
“Hatuwezi kufanya hivyo, Rais hawezi kuomba radhi kwa kitendo hiki….hawezi kuomba radhi kwa kitendo hiki, wafanye mazungumzo na kwamba Tanzania itatoa ushirikiano,” alisema.
AJIGAMBA KUIMWAGA MALAWI KUHUSU ZIWA NYASA
Kuhusu mgogoro wa mipaka kati ya nchi ya Malawi na Tanzania, Membe alisema wamejiandaa kwa ushahidi wa kutosha chini ya jopo la wanasheria wakiongozwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Mgogoro huo ambao Malawi wanadai kuwa Ziwa Nyasa ni mali yao, sasa unatatuliwa na marais wastaafu wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (Sadc).
“Tumejiandaa tuna ushahidi kama mlima wa Kilimanjaro sasa hatuwezi kusema hapa tumejiandaaje? Lakini hashindwi mtu, maji yale ni yetu,”alisema.
Alisema kama Msumbiji ilikwenda kudai maji ya Ziwa Nyasa na ikashinda sembuse kwa Tanzania na kuhoji kwanini isishinde.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
No comments:
Post a Comment