RAIA wa Uingereza anayeendesha klabu cha usiku eneo la Mtwapa ameshtakiwa katika mahakama ya Shanzu kwa kuwafanya wanawake tisa kucheza densi wakiwa
uchi mbele ya wateja wake ili kujinufaisha kifedha.
Bw Ian Huthson ambaye alikamatwa Jumapili usiku alikanusha kuwatumia wasichana hao katika ukahaba mbele ya hakimu mkaazi James Ombura.
Baadhi ya wasichana tisa waliokamatwa katika jumba la burudani la Banoff, Mtwapa, Kaunti ya Kilifi wakiwa katika mahakama ya Shanzu ambapo walishtakiwa kwa kucheza densi wakiwa uchi Juni 3, 2013.
Mwendesha Mashtaka Paul Makonge aliomba mahakama kuwa mshukiwa azuiliwe hadi Jumanne ili kupatia polisi muda wa kubainisha ikiwa alikuwa na kibali cha kufanya kazi nchini.
“Mheshimiwa hakimu, mshukiwa alikamatwa usiku na tunauliza mahakama kuwa kesi itajwe kesho (Jumanne) kwa sababu tunahitaji kubainisha ikiwa ana leseni ya kufanya biashara,” alisema Bw Makonge.
Pia upande huo wa mashtaka ulisema unahitaji kuchunguza stakabadhi nyingine muhimu kuhusiana naye Bw Huthson kabla aachiliwe kwa dhamana.
Ilidaiwa kuwa mnamo Juni 3, 2013 katika klabu cha Banhof mjini Mtwapa, akiwa mmiliki wa klabu na kwa matarajio ya kujinufaisha kifedha yeye binafsi na wanawake hao tisa, aliwasimamia kucheza densi uchi, ambayo ilihusiana na ukahaba wa washukiwa.
Wanawake hao tisa walioshtakiwa kando, walikiri shtaka la kuendesha shoo isiyofaa.
Washukiwa hao walikuwa Wanjiku Kamau, Mwanajuma Hamis, Sylver Otieno, Immaculate Koni, Sofia Koni, Ann Wangari, Samanja Hassan, Stephen Maina na Veronica Ogola.
Mahakama iliidhinisha ombi la Bw Makonge kuruhusiwa kuwasilisha maelezo kuhusu mashtaka yao Jumanne kabla ya kuhukumiwa.
“Afisa wa upelelezi pia bado hajachukua alama za vidole kutoka kwa washukiwa na tunaomba muda wawekwe rumande hadi kesho ili tuweze kusomea mahakama maelezo ya mashtaka,” upande wa mashtaka ulisema.
Washukiwa hao walifikishwa mahakamani huku wanawake wengine waliobeba mabango wakifanya maandamano ya amani kuitaka serikali ichukue hatua dhidi ya vilabu vingine vya usiku vinavyodaiwa kuhusika na matukio sawa na hayo.
Katibu wa tawi la Mtwapa la Shirika la Maendeleo ya Wanawake (MYWO), Bi Mufida Mohammed alitaka wageni wanaodaiwa kuendesha dhuluma dhidi ya watoto watimuliwe.
Naibu mwenyekiti wa Baraza la Maimam na Wahubiri Kenya (CIPK) tawi la Kilifi, Sheikh Ali Hussein alipongeza polisi kwa hatua ya haraka kuzuia shoo hiyo na kuomba serikali kuwatimua wageni wanaodaiwa kuhusika katika biashara za aina hiyo.
Pia aliuliza bodi ya kutoa leseni za vileo kufuta leseni zilizotolewa kwa vilabu vya usiku katika mji huo wa watalii.
“Wageni hao wanafahamika kwa kuendesha biashara chafu na tunataka wakamatwe na kushtakiwa,” aliongeza.
Sodoma
Askofu Launce Chai wa Baraza la Kitaifa la Makanisa Kenya (NCCK) alisema wasichana wachanga ambao ni pamoja na walio shule wanahusika katika biashara hiyo ya kucheza uchi vilabuni Mtwapa.
“Kinachoendelea katika mji huu hakikuwahi kutokea katika enzi ya Sodoma na Gomora. Tunawatahadharisha wageni wote na wafuasi wao wa humu nchini wanaohusika na shoo za ngono,” alisema.
Pia walitaka mwanamume aliyetambuliwa kama Spider Man ambaye alitoroka wakati wa msako huo akamatwe.
Wakati huo huo, Kamishna wa Kaunti ya Kilifi Erastus Ekidor alisema baadhi ya wanawake waliokamatwa ni wachanga na walikuwa wameshawishiwa kuingia kwa ukahaba.
Pia alisema kuwa polisi wanachunguza vilabu sita Mtwapa na Malindi ambapo kumedaiwa kuwa na shoo hizo za ngono.
No comments:
Post a Comment