RAIS Jakaya Kikwete, amewasiliana na Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, ili azungumze na Rais wa Rwanda, Paul Kagame kwa nia ya
kumaliza mvutano wa maneno kati yao kwa busara.
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alisema hayo jana bungeni, alipokuwa akijibu swali la Kiongozi wa Upinzani bungeni, Mbunge wa Hai, Freeman Mbowe (Chadema).
“Tunataka suala hili limalizike kwa njia ya busara, ili watu waendelee kuchapa kazi, ninaamini busara zitatumika kumaliza tatizo hilo,” alisema.
Akiuliza swali katika kipindi cha maswali ya Papo kwa Hapo kwa Waziri Mkuu jana, Mbowe alitaka kujua kauli ya Serikali na mikakati iliyopo kupata suluhu katika mvutano wa maneno uliojitokeza kati ya Rais Kikwete na Rais Kagame.
Pia Mbowe alitaka Serikali kuunda jopo la ushawishi wa kimataifa, kutokana na Rwanda kuonekana kushawishi nchi za Uganda na Kenya, jambo ambalo linaashiria kuitenga Tanzania katika shughuli mbalimbali za Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Kwa mujibu wa Mbowe, kitendo cha marais wa Kenya, Uganda na Rwanda kukutana katika mikakati ya kuanza kutumia bandari ya Mombasa ambayo ingekuwa ya nchi za Afrika Mashariki, ni dalili kuwa Tanzania imeanza kutengwa.
Mbowe alisema pamoja na kuanza kutengwa kwa Tanzania katika shughuli za Afrika Mashariki pia kumekuwa na mgogoro uliozuka hivi karibuni wa Bunge la Afrika Mashariki, kutaka vikao vya Bunge hilo vifanyike kwa kupokezana katika nchi wanachama, tofauti na ilivyokuwa awali, ambapo vikao hivyo vilifanyika Arusha.
Hata hivyo, Pinda katika jibu lake, alisisitiza kuwa hakuna sababu ya Serikali kuunda jopo la kutafuta ushawishi wa suluhu na Rwanda kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), kwa kuwa hakuna sababu za kufanya hivyo.
Hakuna uhasama Akifafanua, Pinda alisema Serikali haina sababu ya kujenga uhasama na Rwanda, kwa kuwa nafasi ya Tanzania na mchango wake katika nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu na Afrika unajulikana.
Alisisitiza, kuwa ushauri aliotoa Rais Kikwete wa kutaka Rwanda kukaa meza moja na waasi, ulikuwa wa busara na haukuwa na tatizo lolote.
Kutokana na msingi huo, alifafanua kwamba ndiyo maana Tanzania haiangalii mvutano huo wa maneno kama tatizo, ingawa Serikali haitapuuza suala hilo linaloonesha kuwepo kwa dalili ya kutoelewana.
“Ukilitazama suala hili huwezi kuamini kama kweli kauli ya Rais Kikwete ingeleta haya, nadhani wenzetu wanalitazama kwa namna tofauti na sisi tunavyolitazama,” alisema.
Pinda alirejea kiini cha mtafaruku huo, kuwa ni ushauri wa Rais Kikwete kwa nchi ya Rwanda kukaa meza moja na waasi, ili kuacha mapigano kwa maslahi ya wananchi wa Rwanda.
Alisema kauli hiyo iliyotolewa na Rais Kikwete katika mkutano wa Umoja wa Afrika (AU) uliofanyika Ethiopia, ilikuwa na nia njema kwa maslahi ya Rwanda, lakini imechukuliwa tofauti nje ya mkutano huo.
Propaganda za biashara
Katika hatua nyingine, Naibu Waziri wa Uchukuzi, Dk Charles Tizeba, alisema kauli zinazotolewa kuwa mizigo ya Rwanda haitapitishwa kwenye bandari ya Dar es Salaam, ni propaganda za kibiashara kutoka nchi washindani.
Hata hivyo, Dk Tizeba hakuwa tayari kubainisha ni nchi ipi inahusika zaidi kutoa propaganda hizo ingawa aligusia kwamba ni nchi zenye bandari.
Alisema baada ya kukutana na wafanyabiashara wa Rwanda na viongozi wa Serikali ya nchi hiyo, wamebaini kuwa hakuna upande uliozuia mizigo kupita Tanzania.
“Huku wanasema kuna maelekezo kwamba wafanyabiashara wa Rwanda wasipitishe mizigo Tanzania, lakini kwa Rwanda wao wanasema Tanzania imezuia mizigo ya Rwanda kupita Tanzania … tumebaini kuwa kauli hizi hazikuwa na ukweli,” alisema.
Alisema wafanyabiashara wa Rwanda wamesema kama Tanzania wanataka Rwanda ipitishe mizigo mingi, ifanye marekebisho kadhaa, ikiwemo kukabiliana na matatizo kama lililowahi kutokea la kupotea kwa kontena mbili za dhahabu na mbolea, kuangalia tozo za kusafirisha magari yasiyosajiliwa Tanzania na kupunguza wingi wa mizani ambao wanadai unachelewesha usafirishaji.
Pia Tizeba alisema walilalamikia udokozi wa vitu vidogo kwenye magari bandarini, jambo ambalo limefanyiwa kazi na hali hiyo haipo tena, kwani baadhi ya magari vifaa vyao vilikuwa vikiibwa maeneo mengine kabla ya kufika Dar es Salaam.
“Kuna mambo mengi yanafanyiwa kazi ikiwamo kuwa na treni mbili za mizigo hadi Isaka, ambazo zitasafirisha mizigo ya Rwanda, Kongo na Burundi, na pia kuweka ofisa wa bandari Kigali, ambaye atakuwa akishughulikia matatizo na kuanzisha mizani ambayo itapima gari likiwa linatembea na kuwa na mizani maeneo matatu,” alisema.
Kuhusu hatua ya Rais Kagame kuzindua mpango wa nchi yake kutumia bandari ya Mombasa, Tizeba alisema nchi inaweza kuwa na njia nyingi za kupitishia mizigo, na kubainisha kuwa bado Tanzania ndilo eneo pekee zuri kwa kusafirisha mizigo kwa nchi zisizo na bandari.
HABARILEO AGOSTI 30, 2013
No comments:
Post a Comment