Find us on facebook

Pages

Follow Me.

Monday, August 5, 2013

SITTA ASEMA WABUNGE VITI MAALUMU HAWANA UMUHIMU WOWOTE.

Asema wengi hawachangii lolote bungeni na hawana yeyote wa kuwahoji kama ilivyo kwa wale wa majimbo.

*Aunga mkono Rasimu ya Katiba Mpya kufuta viti hivyo, asema ni mzigo mwingine kwa wananchi.
Dar es Salaam. 

Wiki moja baada ya kukaririwa akisema baadhi ya wabunge wa CCM ni mizigo na kwamba hawana mchango wowote bungeni na wala

hawatembelei majimbo yao wakisubiri kubebwa na chama, Spika wa Bunge wa zamani, Samuel Sitta amewageukia wabunge wa Viti Maalumu akisema hawana umuhimu wowote.

Akizungumza kwa simu juzi, Sitta ambaye sasa ni Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki alisema: “Ninakerwa sana na mfumo wa Viti Maalumu, kwanza sioni umuhimu wa mfumo huu kuendelea kuwepo katika Katiba Mpya. Hawana umuhimu wowote.”

Katika mkutano wake wa hadhara uliofanyika Uwanja wa Shule ya Msingi Nyamikoma, Kata ya Busega Mkoa wa Simiyu Julai 29, mwaka huu ikiwa ni sehemu ya kampeni za kuimarisha uhai wa chama, Sitta aliwajia juu bila ya kuwataja baadhi ya wabunge wa CCM.

“Wanakwenda bungeni hawachangii, hawana hata hoja za kuchachafya upinzani, hawachangii, hawa ni mzigo,” alisema Sitta na kuongeza: “Wapo baadhi ya wabunge, hawajawahi hata siku moja kwenda kwenye majimbo yao kuwatembelea wananchi waliowachagua... Inawezekana hata wapiga kura wakawa wamewasahau. Hawa hawafai hata kuchaguliwa wakiomba tena kura.”

“Rais Jakaya Kikwete amejitahidi sana kuleta mabadiliko, ameleta mafanikio ya uchumi na mambo mengi. Inatakiwa wabunge waende wakawaeleze wananchi maendeleo haya, inawezekana hawayajui lakini watu hawaendi jimboni, wananchi watayafahamu vipi haya maendeleo?”

Juzi, akizungumzia wabunge wa Viti Maalumu, Sitta alisema... “Wengi wao hawachangii chochote na mbaya zaidi hakuna wa kuwahoji chochote kama wabunge wanavyorudi jimboni.

“Ikifika wakati wa posho wapo. Sisemi kama naumia wao kuchukua posho.... hawa wanachukua posho wanawajibika kwa nani? Nani anahoji utendaji wao na zaidi itakapokuja Katiba Mpya ya kuwawajibisha wabunge wazembe, hawa watawajibishwa wapi?”

“Rasimu ya Katiba Mpya isiwaruhusu hawa... hawa nao ni mzigo mwingine. Wakifika bungeni hawachangii chochote, hawawezi kuwajibishwa na yeyote kwa mfumo uliopo na pia hawawajibiki popote, sasa huu si mzigo?”

Walikwishaanza mkakati

Hata hivyo, Juni 9, mwaka huu, ikiwa ni wiki moja baada ya Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba kutangaza Rasimu ya Katiba huku ikifuta Viti Maalumu, wabunge wanawake walianza kuweka mikakati ya Uchaguzi Mkuu wa 2015 kwa lengo la kukamata majimbo.

Kwa mara ya kwanza, wabunge hao wa Viti Maalumu walikutana kwa siku mbili kwenye Ukumbi wa Pius Msekwa, Dodoma lengo likiwa ni kujadili mikakati mbalimbali ya kupambana jimboni.

Mwenyekiti wa Wabunge Wanawake, Anna Abdallah alisema wanaweka mikakati kuwawezesha kusimama wenyewe kwenye majimbo mwaka 2015 hasa baada ya kufutwa kwa Viti Maalumu katika rasimu.
Source: Mwananchi

No comments:

Post a Comment