Find us on facebook

Pages

Follow Me.

Friday, May 31, 2013

CCM NA MBINU ZA KUHUJUMU UBUNGE WA LISSU

Mnadhimu Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni na Mbunge wa Singida Mashariki (CHADEMA), Tundu Lissu, amekaliwa “kooni’ tena, kufuatia hatua ya
makao makuu ya CCM, kuagiza mawakili kukata rufaa Mahakama ya Rufaa nchini kupinga uamuzi wa mahakama kuu kanda ya Dodoma uliotupilia mbali kesi ya uchaguzi mwaka jana.

Taarifa za kuaminika na zilizothibitishwa na Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa zimedai kwamba CCM imewaelekeza waliowakuwa mawakili wa makada wa CCM waliomfungulia Lissu kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa ubunge katika jimbo la Singida Mashariki mwaka 2010 wakate Rufaa Mahakama ya Rufaa ya Tanzania ili kupinga uamuzi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Dodoma iliyotupilia mbali kesi hiyo Aprili 27, mwaka jana.

Kwa mujibu wa barua kutoka kwa kampuni ya uwakili iliyoandaliwa Katibu Mkuu wa CCM barua yenye kumbu kumbu Na. NO/KM/CCM/01/2013 yenye kichwa cha maneno kisemacho: “MADAI YA MALIPO YA AWALI YA SHAURI LA RUFAA KESI YA UCHAGUZI JIMBO LA SINGIDA MASHARIKI SHABANI ITAMBU SELEMA NA MWENZAKE DHIDI YA MH. TUNDU LISSU” rufaa dhidi ubunge wa Lisu imefunguliwa.

Barua hiyo inamkumbusha Katibu Mkuu wa CCM, juu ya ‘makubaliano’ kati ya Wassonga Associates Advocates na CCM kuhusu kusimamia kesi ya wanachama hao wa CCM dhidi ya Lissu.

“Baada ya shauri husika nilipata maelekezo kutoka kwa wanasheria wa CCM kwamba tukate rufaa Mahakama ya Rufaa kazi ambayo tumekamilisha.” Wakili Wassonga anamweleza katibu mkuu: “... katika shauri la mwanzo nilikuwa nalipwa na CCM Singida Mkoa na hawakumalizia malipo.” Barua hiyo imeambatana na hati ya madai ya malipo (invoice) kwa ajili ya ‘malipo ya awali’ ya shilingi milioni mbili.

Akizungumza jana na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Dk. Slaa alisema hatua hiyo ya CCM, imelenga kuhakikisha Lissu anafutiwa ubunge ili asishiriki katika mchakato wa Katiba mpya kama mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba litakalojadili na kupitisha rasimu ya Katiba mpya baadaye mwaka huu.

“Kwa kipindi kifupi ambacho amekuwa Mnadhimu Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni na Mbunge, Lissu, amekuwa mwiba mkali kwa CCM na serikali yake ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano. Amefumbua macho ya mamilioni ya Watanzania kuhusu masuala makubwa ya Kikatiba na kisheria kwa hoja zake bungeni.

“Uelewa wake mpana wa masuala hayo na Kanuni za Bunge umekuwa kikwazo kikubwa kwa CCM na serikali yake pamoja na uongozi wa Bunge kupitisha mambo yao kinyume cha sheria, kanuni za Bunge na maslahi ya nchi yetu. Uwepo wake ndani ya Bunge na ujasiri wake katika kutetea hoja mbalimbali umemzuia Spika wa Bunge na uongozi mzima wa Bunge kuwaonea wabunge wa upinzani na hasa wa CHADEMA. Mtu huyu amekuwa adui mkubwa wa CCM ndio maana Kinana anataka aondolewe bungeni ili asiwepo kabisa katika mjadala wa Katiba mpya bungeni.”

Ijapokuwa rufaa hiyo inaonyesha kufunguliwa na Shabani Itambu Selema na Paschal Marcel Hallu waliokuwa walalamikaji katika kesi iliyotupwa na Mahakama Kuu, Dk. Slaa alidai kwamba watu hao hawahusiki kwa namna yoyote ile na kufunguliwa kwa rufaa hiyo.

“CCM na mawakili wao wanawatumia tu wanakijiji hawa bila hata kuwapa taarifa au kuwashirikisha kwa namna nyingine yoyote. Huyu Shabani Itambu Selema amekula kiapo mahakamani Dodoma kwamba yeye na mwenzake ambaye bado ni Katibu Kata wa CCM huko kwao, hawakuambiwa chochote juu ya kufunguliwa kwa rufaa hiyo.

“Hawakutoa maagizo yoyote kwa Wakili Wassonga kufungua rufaa kwa niaba yao dhidi ya Lissu; hawajamruhusu Wakili huyo kupinga maamuzi ya Mahakama Kuu iliyoridhika kwamba uchaguzi wa Mbunge Lissu ulikuwa halali; hawajamlipa Wakili Wassonga kwa ajili hiyo,” alisema Dk. Slaa.

Dk. Slaa alidai kwamba kazi ya Lissu na wabunge wa CHADEMA ndani ya Bunge inawatisha CCM na serikali yake ndio maana sasa CCM inataka Lissu aenguliwe kwa kutumia Mahakama ya Rufaa ya Tanzania.

“CCM inatapatapa, bungeni hapakaliki kwa sababu ya hoja za Lissu na wabunge wengine wa CHADEMA. Kila siku Bunge linaahirishwa ili kukwepa mijadala mikubwa juu ya matukio muhimu yanayoisibu nchi yetu. Njama za kuizima CHADEMA kwa kuipunguzia muda wa kuzungumza bungeni zimeshindikana; mikakati ya kuvuruga hoja za CHADEMA kwa kuingilia hotuba za Kambi Rasmi ya Upinzani na kutaka sehemu za hotuba hizo zifutwe zimegonga mwamba; vitisho vya Spika Makinda na Naibu Spika Ndugai kuwasimamisha wabunge wetu hazijafua dafu..”

Akizungumzia hati ya kiapo ya Shabani Itambu Selema ambaye alihama CCM na kujiunga na CHADEMA baada ya kesi yao kutupiliwa mbali na Mahakama Kuu mwaka jana, Dk. Slaa alisema: “Tutaishangaa sana Mahakama ya Rufaa kama itaisikiliza rufaa hiyo hata baada ya aliyekuwa mhusika wa kesi ya msingi kusema kwa kiapo kwamba yeye na mwenzake hawajakata rufaa bali ni mambo ya CCM!

“Kwa mujibu wa kifungu cha 115 cha Sheria ya Uchaguzi, Sura ya 343, Mahakama ya Rufaa inatakiwa kusikiliza rufaa dhidi ya uamuzi wa Mahakama Kuu ndani ya kipindi cha mwaka mmoja tangu rufaa ilipofunguliwa. CCM wamesubiri mwaka umepita tangu Mahakama Kuu ilipokataa kufuta matokeo ya Lissu ndio wafungue rufaa. Kama huku sio kukanyaga spirit ya sheria hiyo ni kitu gani?” alihoji Dk. Slaa.

Aliongeza kuwa katika kesi ya Mbunge wa Arusha Mjini (CHADEMA), Godbless Lema, aliyekuwa anashtakiwa na wana CCM pia, Mahakama ya Rufaa ilipiga marufuku wapiga kura ambao hawakunyimwa haki zao za kupiga kura kufungua malalamiko ya kupinga matokeo ya uchaguzi mahakamani.

“Hata wino wa Mahakama ya Rufaa katika hukumu ya Lema haujakauka CCM wanataka Mahakama ya Rufaa ile matapishi yake kwa kusikiliza rufaa ya wapiga kura wanaodai kwa kiapo kwamba walielekezwa na wakubwa wao katika CCM kufungua kesi iliyokataliwa na Mahakama Kuu na sasa rufaa imefunguliwa bila hata wao kujulishwa au kushirikishwa kwa namna yoyote ile.”

Dk. Slaa alisema kwamba rufaa ya sasa inathibitisha kauli inayodaiwa kutolewa na Rais Jakaya Kikwete juu ya Tundu Lissu wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu uliopita ambapo Kikwete alidaiwa kuwaambia wana CCM mjini Singida kwamba ni afadhali Dk. Slaa achaguliwe kuwa Rais kuliko Tundu Lissu kuwa mbunge!

“Kwa kazi zake ndani na nje ya Bunge Lissu amethibitisha umahiri na uzalendo wake kwa Tanzania na kwa chama chetu. Ametetea wabunge na viongozi wetu dhidi ya njama za CCM kuwachafua kwa kuwafungulia mashtaka ya uongo mahakamani; ametetea Watanzania kila mahali nchini, na ameelimisha wananchi kwa hoja zake bungeni. Ni mmoja wa wabunge hodari, jasiri na wachapa kazi katika Bunge hili. Huyu ndiye mbunge ambaye CCM wanataka aondolewe bungeni kwa mbinu za kishetani za aina hii. Hatutakubali na tunawataka Watanzania wasikubali!”

Rufaa dhidi ya Lissu bado haijapatiwa namba ya usajili licha ya kwamba imeshalipiwa ada ya kuifungulia na tayari imeshapokelewa na Masjala Ndogo ya Mahakama ya Rufaa ya Tanzania, Dodoma. Aidha, rufaa hiyo haijapangiwa majaji wa kuisikiliza wala tarehe ya kusikilizwa kwake haijapangwa.


Chanzo: Tanzania Daima

No comments:

Post a Comment