Find us on facebook

Pages

Follow Me.

Sunday, June 30, 2013

EMMANUEL OKWII SASA KUUZWA ULAYA

Dar es Salaam. Klabu ya Etoile du Sahel ya Tunisia inatarajia kumpiga bei mshambuliaji wake, Emmanuel Okwi kabla hata haijamaliza malipo ya deni la kumnunua mchezaji huyo raia wa Uganda kutoka Simba ya Dar es Salaam.
Okwi, aliyenunuliwa na Simba kutoka Sports Club Villa ya Uganda mwaka 2010 kwa ada ya uhamisho ya Dola 40,000, anatarajiwa kuuzwa klabu ya
FK Partizan ya nchini Serbia.
FK Partizan inayocheza Ligi Kuu, maarufu kama SuperLiga inashika nafasi ya pili kwa ukubwa na mafanikio ya jumla, kiuchumi na uwanjani Serbia tangu ilipoanzishwa mwaka 1945.
Taarifa za klabu ya Etoile du Sahel kumuuza Okwi aliyecheza kwa mafanikio Msimbazi, zilithibitishwa jana na Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zakaria Hanspope.
“Ni kweli, Okwi anaweza kuuzwa Ulaya na sisi hatuna namna ya kumzuia hata kama bado Etoile du Sahel haijatulipa pesa za kumnunua kutoka kwetu,” alisema Hanspope.
Pope alisema kama hatua ya kuuzwa mchezaji huo itatimia, basi itakuwa neema kwao kwani makubaliano yanaonyesha, kama ikitokea klabu hiyo ya Tunisia ikamuuza Okwi, basi Simba itapata asilimia 25 ya mauzo.
Hanspope pia alisema kuwa, kama Okwi atauzwa basi maana yake klabu hiyo ya Tunisia italipa pesa mara moja wanazodaiwa za kumnunua mchezaji huyo mwaka jana, ambazo Sh450 milioni.
“Makubaliano yetu ya kuuzwa Okwi ni kwamba, klabu hiyo ya Tunisia itatulipa pesa kwa awamu, lakini kama itatokea na wao wakamuuza basi pesa zetu tutalipwa mara moja,” alifafanua Hanspope.
Okwi alionyesha kiwango kizuri kilichowavutia kocha wa klabu hiyo ya Serbia, Vuk Rasovic na Mkurugenzi wake Albert Nagy wakati akiichezea Uganda dhidi ya Angola katika mchezo wa kuwania kufuzu kucheza fainali za Kombe la Dunia mwaka.
Taarifa zilizopatikana kwenye tovuti, zimeeleza kuwa mazungumzo kati ya pande hizo mbili yameshaanza na yanasimamiwa kwa karibu na Kocha wa Timu ya Taifa ya Uganda, Sredojevich ‘Micho’ Milutin.
Mbali na Simba pia timu yake ya Sports Club Villa ya Uganda itanufaika na mgawo huo wa mauzo ya Okwi kutokana na kukuza kipaji chake toka akiwa mchezaji chipukizi.
Kwa upande wa Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hanspope alipoulizwa alisema hana pingamizi lolote la kuuzwa kwa mshambuliaji huyo zaidi ya kupaswa kulipwa fedha zao kihahali kwa mujibu wa kanuni.
CHANZO:MWANANCHI

No comments:

Post a Comment