Mwanamume aliyefichua habari za ujasusi za Marekani, akiwa Hong Kong, sasa ametoweka hotelini mwake. Edward Snowden aliambia waandishi wa habari kuwa
ameishiwa na pesa na alisema ana hakika kuwa maafisa wa usalama wa Marekani watamtafuta kokote aliko.
Mfanyakazi huyo wa zamani wa CIA, mwenye umri wa miaka 29, aliyekuwa akifanya kazi na CIA alisema kuwa maafisa wa kijasusi wa Marekani walitumia mitambo maalumu kupekua simu, barua pepe na aina nyingine za mawasiliano kote duniani. Alisema kuwa alifichua njma hiyo kwa sababu aliamini ilikuwa kinyume cha demokrasia.
Ikulu ya White House haijasema iwapo itatoa amri ya Edward Snowden kurudishwa nchini ili kushtakiwa kwa kosa hilo. Msemaji wa Ikulu, Jay Carney, alikataa kufafanua ila akaeleza tu kuwa uchunguzi unaendelea na akakariri kuwa kitendo cha Snowden kimehatarisha usalama wa Marekani.
Ingawa kuna wale ambao wamtaja Snowden kama msaliti kwa taifa, kuna wale waliomshangilia kama shujaa wa kitaifa. Maelfu ya watu wametia sahihi katika mtandao wa Ikulu ya White House wakitaka asamehewe kwa makosa yo yote ambayo huenda ameyafanya kisheria.
Huku mjadala ukiendelea iwapo Snowden alifanya kosa au la ni dhahiri sasa kuwa idara ya ujasusi ya Marekani itatafuta njia nyingine ya kukusanya habari zake za kijasusi. Itabidi wajue iwapo kuna watu wengi kuliko inavyodhaniwa wanaofahamu siri za Serikali, ambao wanaweza kuzifichua kwa umma wakati wo wote.
No comments:
Post a Comment