Mkutano wa 11 wa Bunge la Muungano unaendelea leo baada ya mapumziko ya mwishoni mwa wiki, huku wabunge na wananchi wakisubiri Bajeti ya Serikali.
Baada ya wizara 32 kumaliza kuwasilisha makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2013/14, kinachosubiriwa sasa ni
bajeti kuu.
Mwishoni mwa wiki iliyopita, wabunge walikamilisha michakato ya kupitisha maombi ya fedha kila wizara, tayari wizara zote zinasubiri kasma ya Serikali kwa shughuli za kawaida na maendeleo.
Wakati hayo yakiendelea, Kamati ya Bajeti nayo ilikuwa hatua za mwisho kukamilisha kazi yake ya kutengeneza mazingira ya mwelekeo wa bajeti hiyo kabla ya Bajeti Kuu itakayowasilishwa siku nne zijazo.
Katika kuweka sawa hilo, wizara licha ya kuwasilisha makadirio ya mapato na matumizi bungeni kwa mwaka 2013/14, ziliwasilisha kwenye kamati hiyo ili kuona jinsi ya kusaidia na kurahisisha utekelezaji bajeti husika kila wizara na idara zake.
Changamoto kubwa katika utekelezaji bajeti kwa mwaka 2013/14, ni upatikanaji fedha ambazo licha ya kutoka Serikali Kuu, zinategemea fedha za wahisani ili kukamilisha bajeti hiyo.
Katika mkutano huu ambao unaendelea mjini hapa, Bunge lilianza na makadirio ya mapato na matumizi ya wizara zilizo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu na kuhitimisha na Wizara ya Fedha.
Shughuli nyingine ambayo imekwisha kufanyika hadi sasa, ni uchaguzi wa wajumbe katika uwakilishi wa taasisi mbalimbali, vyuo vikuu na Jumuiya ya Uchumi Kudini mwa Afrikaa (SADC).
Kwa utaratibu wa kawaida, Alhamisi asubuhi, Bunge litaanza kwa kupokea taarifa ya hali ya uchumi ambayo itasomwa na waziri mwenye dhamana ya Mipango ya Uchumi kabla ya jioni kusomwa Bajeti Kuu.
Ratiba ya Bunge inaonyesha baada ya kusomwa kwa Bajeti Kuu, siku hiyo mchana Bunge litaahirishwa ili kuwapa nafasi wabunge kuipitia kabla ya Jumatatu wiki ijayo kuanza kujadiliwa kwa siku saba.
No comments:
Post a Comment