KAMANDA wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas, amedai kuwa uchunguzi wa awali kuhusu ujumbe unaodaiwa kutumwa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo, umetumwa na mtandao wa simu wa nje ya nchi.
Kamanda alisema katika ujumbe huo ambao Lema anadai uliandikwa na Mkuu wa Mkoa Mulongo na kutumwa kwenye simu yake Aprili mwaka huu, uchunguzi wa polisi umeonyesha kwamba haukutumwa kupitia kampuni moja wapo ya simu za mikononi ya hapa nchini.
“Katika kipindi cha mwishoni mwa Aprili mwaka huu, vyombo vingi vya habari vikiwemo radio, magazeti na mitandao ya kijamii viliandika na kutangaza habari iliyoelezea shutuma zilizotolewa na Mbunge Lema kuwa aliandikiwa ujumbe wa vitisho kwa njia ya simu na Mkuu wa Mkoa Mulongo na ulisomeka:
“Umeruka kihunzi cha kwanza nitakuonyesha mimi ni serikali, ulikojificha nitakupata na nitakupa kesi inayoitaka mimi.”
Kamanda Sabas alisema ujumbe huo ulidaiwa kutumwa kutoka namba 0752960276 inayotumiwa na Mkuu wa Mkoa Mulongo kwenda kwenye namba 0764150747 inayotumiwa na Lema. Alisema kufuatia tuhuma hizo, polisi walianza uchunguzi kwa kuzingatia kuwa Mulongo alikanusha kutuma ujumbe wa aina yo yote kwa Mh Lema.
Alisema uchunguzi huo ulihusisha kampuni ya simu ambayo mtandao wake ulitumika katika utumaji wa ujumbe husika. Alisema uchunguzi wa awali wa polisi umebaini kuwa chanzo cha ujumbe huo mfupi hakikuwa kampuni ya simu husika (hakuitaja) kwa vile ‘Centre Number’ iliyotumika kutuma ujumbe huo mfupi wa maneno ni 44780200332, ambayo siyo ya mtandao wa kampuni husika bali ni ya mtandao ulio nje ya nchi.
Alisema uchunguzi zaidi unaendelea kubaini chanzo cha ujumbe huo mfupi wa simu na mtu aliyehusika kutuma hatua za kisheria zitaweza kuchukua mkondo wake.
No comments:
Post a Comment